MAN CITY, YACHUKUA KOMBE LEO TAZAMA - Smartdesmarttz

BELIEVE WHAT YOU HAVE(MWANZO MGUMU)

Jumapili, 6 Mei 2018

MAN CITY, YACHUKUA KOMBE LEO TAZAMA


JURGEN Klopp na Antonio Conte leo Jumapili wanapasuana pale Stamford Bridge, Mourinho yeye anaendelea kulia na wachezaji wake baada ya kuchapwa juzi usiku, lakini kwa Pep Guardiola na jeshi lake la Manchester City ni furaha tupu pale Etihad. Iko hivi. Chelsea na Liverpool zitaonyesha kazi uwanjani Stamford Bridge kwenye mchezo wa Ligi Kuu England utakaokuwa na upinzani mkali, lakini Guardiola yeye atakuwa akikabidhiwa taji lake la kwanza la England mara baada ya mchezo wao dhidi ya Huddersfield Town. Tayari maandalizi ya wachezaji, viongozi na mashabiki wa Man City kupokea ubingwa huo yamepamba moto kwelikweli na nahodha wake Vincent Kompany ndiye atanyanyua kombe hilo kuashiria kuuleta ufalme wa soka la England jijini Manchester. Guardiola, ambaye ataingia uwanjani kuiongoza City akitaka kushinda ili kunogesha sherehe hizo za ubingwa, ataungana na maofisa wa City zaidi ya 500 kusherehekea ubingwa huo. Uwanja wa Etihad utarindima kwa kelele wakati jeshi la Guardiola likikabidhiwa mwali huyo, ambaye amemnasa mapema tu huku wakivunja rekodi kibao na kuweka mpya Kwa sasa Man City ina pointi 93 ikiwaacha mahasimu wao, Man United iliyopo nafasi ya pili kwa pointi 13 hivyo, kuhitaji kushinda mechi zilizobaki ili kujitanua zaidi. Tayari imevunja rekodi ya Chelsea iliyoweka msimu uliopita kushinda michezo 30, ambapo kama ikishinda mechi hizo itakuwa imeshinda mechi 33. Man City pia imeweka rekodi ya kushinda mechi 12 mfululizo msimu huu huku ikiweka rekodi ya kushinda 11 ugenini. Hata hivyo, sherehe hizo zinaweza kwenda sambamba na huzuni pale kiungo wa nguvu na aliyeibeba Man City mabegani kwake kwa muda mrefu na kuipa mataji kibao, Yaya Toure atakapokuwa anaaga mashabiki, wachezaji na viongozi pale Etihad. Kiungo huyo wa kimataifa wa Ivory Coast atatumia fursa hiyo kuaga mashabiki baada ya kumaliza mkataba wake na kuruhisiwa kuondoka akihitimisha miaka nane tangu alipotua akitokea Barcelona. Tayari Guardiola ameahidi kumjumuisha Yaya kwenye kikosi kitakachocheza dhidi ya Huddersfield Town na baadaye kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Brighton Jumatano. Yaya hajaanza kwenye kikosi cha kwanza msimu huu katika Ligi Kuu England na Ijumaa alithibitisha kwamba, ataachana rasmi na miamba hiyo ya Etihad. Hata hivyo, kuna taarifa kuwa Yaya anaweza kuendelea kukipiga kwenye ligi hiyo. “Hatakuwepo nasi msimu ujao, lakini tutampa heshima anayostahili. Atacheza dhidi ya Brighton na hiyo itakuwa moja ya matukio mazuri kabisa kwa ajili ya kumuaga. “Hatuwezi kusahau mchango wa Yaya wakati wa Roberto Mancini, Manuel Pellegrini kwa sababu alikuwa mchezaji muhimu sana na amesaidia kuiletea City mafanikio makubwa,” alisema Guardiola.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni